BASATA LAONYA KUMBI, LAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO
PRESS RELEASE
24/03/2016
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni
msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha wamiliki na
waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa
kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali
vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa utumizi wa kumbi, kuepuka
kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na kuhakikisha
ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao.
Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa
kumbi za sherehe na burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika kumbi
zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu ya Pasaka
ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama
hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida katika biashara
zao kiasi cha kuandaa madisko ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa
ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Aidha, baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa kumbi
kwa msingi huohuo wa kuendekeza faida pasi na kujali maelekezo ya vibali vyao
wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na BASATA.
BASATA kama mtoaji wa vibali vya kumbi za sherehe
na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka
maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa
binadamu hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria
zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa
Pasaka njema na yenye furaha tele.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA
KUITHAMINI
Godfrey
L. Mngereza
KATIBU
MTENDAJI, BASATA
Post a Comment