MBARAKA MWINSHEHE: NDIYE ‘FRANCO WA AFRIKA MASHARIKI’

Machi 17, 1973 Mbaraka akimvisha pete mkewe Amne. Picha kwa hisani ya Kijiwe cha Kitime.



Na Daniel Mbega

MOROGORO kuna vipaji vingi – kuanzia soka, ndondi na muziki. Huko ndiko walikotokea akina Leodgar Tenga, Hashim Kambi, golikipa wa zamani wa Sunderland Mbaraka Salum Magembe, Hassan Mlapakolo, Adam Sabu na wengineo ni baadhi tu ya wanasoka waliotoka Morogoro.
Hivi karibuni tu bondia kutoka Morogoro, Francis ‘Maputo’ Cheka alitwaa ubingwa wa dunia kuonyesha kwamba vipaji vya ndondi vimekuwepo kwa miaka mingi tangu enzi zile za klabu za shule za sekondari za Forest Hill na Mzumbe.
Lakini ukizungumzia muziki, hapo nadhani ndipo mahala pake. Walikuwepo akina Salim Abdallah Yazidu ‘Say’ aliyetamba na bendi za Cuban Marimba na Moro Jazz pamoja na ‘Mfalme’ wa gitaa za solo nchini Tanzania, Mbaraka Mwinshehe Mwaruka. Lakini pia tumeshuhudia wanamuziki wengi wa Bongo Fleva wakiinukia huko kama ‘Mfalme wa Rhymes 2004’ Selemani Msindi ‘Afande Sele’ na akina Mdogo Ditto na Belle 9.
Mafaniko mengi yametokea Morogoro kwenye fani hizo. Tulishuhudia mwaka 1975 wakati Mseto iliponyakua Ubingwa wa Taifa wa kandanda na kumaliza utawala wa timu za Dar es Salaam, mafanikio ambayo yalifikiwa pia na Mtibwa Sugar ya Turiani iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu miaka ya 1999 na 2000.
Lakini, Morogoro ulitangazwa zaidi na Mbaraka Mwinshehe, ambaye pia ndiye alikuwa Alama ya Taifa ya Muziki wa Dansi. Ingawa asili yake ni Mdoe ambaye babu yake Chifu Mwaruka alilowea Uzaramoni huko Mzenga, Kisarawe, lakini walio wengi bado wanaamini kwamba jamaa alikuwa Mluguru.
Wakati Mbaraka anazaliwa Juni 27, 1944 katika Kijiji cha Kingolwira, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro, bendi ya Morogoro Jazz nayo ilianzishwa rasmi mwaka huo ikiundwa na akina Makala Kindamile, Joseph Thomas, Seif Ally, Daudi Ally na Shaaban Mwambe.
Mbaraka alikuwa mtoto wa pili katika familia ya watoto 12 wa Mzee Mwinshehe Mwaruka, aliyekuwa karani katika mashamba ya mkonge pale Kingolwira. Nduguze ni Said, Kapita, Halima, Zanda, Zawadi, Matata, Nassibu, Almasi, Mwereka, Kate na Mwazaina.
Mapenzi yake katika muziki yalimfanya Mbaraka akatishe masomo katika kidato cha tatu kwenye shule ya sekondari Mzumbe. Tangu utotoni alikuwa napenda kuimba.
Aalianza kushiriki maonyesho ya bendi ya Moro Jazz akiwa shule, ambapo alipenda kupiga filimbi. Mwaka 1965 wakati waimbaji wa Moro Jazz wakiwa wanabarizi nje ya klabu yao, Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa. Kumbe tayari alikuwa ameondoka shule na alikuwa anaelekea Dar es Salaam ‘kutafuta maisha’. Wanamuziki hao wakamsihi ampumzike atafakari kwanza.
Hata hivyo, kesho yake walipoamka wakamkuta Mbaraka anapiga gitaa, ala ambayo hawakuwahi kumuona akiipiga zaidi ya filimbi yake.
Huo ndio ukawa mwanzo way eye kujiunga na bendi hiyo kwani alifundishwa kupiga rhythm kwa vile hawakuwa na mpigaji. Safari ya Dar ikaishia hapo.
Inaelezwa kwamba kuna siku walialikwa Dar es Salaam ili kushinda na Kilwa Jazz ya Ahmad Kipande. Kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi. Wakati huo waliokuwa wanalipwa kwa mwezi ni wapiga ala hasa gitaa la solo, saxophone na trumpet, wengine wote walikuwa wanapewa posho kila walipopiga dansi.
Baada ya kugoma wazee wa bendi wakakubali kumlipa Shs. 120 kwa mwezi, uamuzi ambao ulimkasirisha mpiga solo aliyekuwa akilipwa Shs. 150 ambaye aligoma kwenda Dar kwa kutetea kuwa mpiga rhythm hastahili malipo.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Mbaraka akasema angepiga pia solo. Viongozi wa bendi walistaajabu kwa sababu Mbaraka hakuwahi kupiga solo kabla na kwa vile Kilwa Jazz wakati huo ilikuwa tisho, walihisi kwamba wangeumbuka. Walipokwenda huko Mbaraka alidhihirisha kwamba alikuwa ‘mchawi wa gitaa’ baada ya kulikung’uta solo vili na bendi yao ikapata ushindi. Badala ya kulipwa Shs. 120, sasa wakampandishia mshahara hadi Shs. 250 kwa mwezi, ambazo zilikuwa nyingi mno wakati huo na tangu hapo akawa mpiga solo hadi alipoondoka mwaka 1973 kuanzia bendi yake ya Super Volcano.

KUHAMA…
Tofauti na sasa, zamani lilikuwa ni jambo geni kwa wanamuziki kuhama bendi moja bila mpangilio. Oktoba 1973 Tanzania ilishuhudia kupanda kwa bei ya mafuta kwa mara ya kwanza. Hali hiyo ikafanya shughuli nyingi za uchumi kuyumba.
Bendi za dansi ambazo zilitegemea kufanya maonyesho ili kujipatia fedha zikashuhudia kuporomoka kwa uchumi baada ya kuwa zikipiga kwenye kumbi zilizo tupu kwa sababu watu hawakuwa na fedha, hata zile kidogo walizokuwa nazo, hawakuwa tayari kuzitumia ovyo.
Ni katika kipindi hiki ambapo Mbaraka aliona ni vyema akatafuta malisho bora, lakini angekwenda wapi? Akaamua kuanzisha bendi yake ya Super Volcano. Hatimaye akaelekea Kenya, akiwa na baadhi ya wanamuziki, japokuwa siyo katika kundi zima kwa sababu mabadiliko ya uchumi yalikuwa yametokea pia Kenya.
Mbaraka akaanza kuutangaza muziki wa Tanzania huko wakati akisaidia kuubadili muziki wa Kenya.

MAPENZI NA MWANAJAMII…
Hakuna shaka yoyote kwamba Mbaraka Mwinshehe ataendelea kuwa utambulisho wa muziki wa dansi Tanzania na nje ya mipaka yake, ndiyo maana wengi walimwita ‘Franco wa Afrika Mashariki’ (Franco of the East Africa) na wengine wakamwita ‘Mchawi wa Solo’.
Jamaa alijua kutunga na jamii inathibitisha hili kila nyimbo zake zinapopigwa. Alijua namna ya kutafuta visa na kuvipangilia, vingi vikiwa ni vya kweli.
Nyimbo kama Mtaa wa Saba, Shida, Jogoo la Shamba, Choyo Uache, Dk. Klerruu, Masimango, Mapenzi Shuleni, Urafiki Mwisho wa Mwezi, Kazi Ndio Msingi, zinazungumzia masuala ya jamii.
Katika nyimbo za Hallo Betty, Dawa Ya Mapenzi, Niliota Ndoto, Amina Mpenzi, Yameshanichosha, Talaka, Nashangaa, Mapenzi Yanitesa, Tutakuja Gombana, Esta Wangu, Pole Dada, Daktari Ni Mimi, Wanisikitisha Mpenzi, Nikupendeje, Nirudie Mama, Roho Ndiyo Mwamuzi, Kasema Hakutaki, Dina Uliapa, Tina Turudiane, Dawa Ya Mapenzi, Penzi Lako Hatari, Mashemeji Wangapi, Tunachogombea Nini, na nyingizo zinazungumzia mapenzi na nyingi kati ya hizo ni visa vya kweli vilivyomtokea ama yeye au wanajamii wengine.
Wimbo wa ‘Mshenga’ unatajwa kuwa ni kisa cha kweli alichotunga kumuelezea mchumba wake ambaye alikuja kuwa mkewe. Pia aliwahi kumtungia mchumba wake huyo nyimbo za ‘Tunachogombea Nini’ na ‘Walisema’ kufuatia maneno ya ‘umbeya’ waliyoyasikia.
‘Jogoo la Shamba’ ni kisa cha kweli baada ya Mbaraka, mkewe na shemeji yake kufanyiwa fujo na fundi cherehani mmoja mjini Morogoro, ambapo mdogo wake Mbaraka aliyeitwa Zanda alimtwanga fundi huyo mwenyeji wa Ulanga, ambako ni ‘shamba’.

MWANAHARAKATI…
Mbaraka hakuwa mwanasiasa, bali mwanaharakati. Alihimiza shughuli nyingi za maendeleo kupitia nyimbo zake kama vile Furaha Ya Saba Saba, Vijana wa Afrika, Mapenzi Shuleni, Mama Chakula Bora, Makao Makuu Dodoma, Matamko Ya Viongozi Wetu, Expo 70 Pt 1 & 2, Watalii, Twawapongeza Wanasoka, Kazi Ndiyo Msingi, Heko U.W.T., Mwongoza Wa Tanu, Ukombozi Wa Afrika, Ujamaa Na Kujitegemea na Poleni Rufiji.
Mwanamuziki huyo aliing’arisha Tanzania kwenye Maonyesho ya Kimataifa nchini Japan mwaka 1970 (Japan Expo 70) kutokana na nyimbo zake, wakati huo akiwa na Moro Jazz.

NDOA…
Machi 17, 1972 Mbaraka alifunga ndoa na Amne Kadribaksh Shahdad, ambaye walibahatika kuzaa naye watoto wawili Masiku anayeishi Afrika Kusini na dada yake Muhitaji ‘Taji’, ambaye anaongoza bendi ya Orchestre Super Volcano akiwa mtunzi, mwimbaji na mpiga gitaa la bass.

MAUTI YAMFIKA…
Bendi nyingi za Tanzania zilikuwa na kawaida ya kurekodi nyimbo zao Kenya ambako walikuwa wamepiga hatua tofauti na Tanzania, ambako walitegemea zaidi Studio za Radio Tanzania pekee.
Mwaka 1978 mwishoni Mbaraka alikuwa Mombasa akiwa na kundi lake la Super Volcano, lengo likiwa kurekodi nyimbo zao. Mbaraka alikuwa amekwenda na familia yake, huku binti yake Muhitaji akiwa na miaka miwili kasoro.
Januari 12, 1979 Mbaraka, akiwa kwenye gari la rafiki yake Omari Abdi wa Moshi aliyekuwa akiendesha, pamoja na mtu mwingine, waliondoka kwenye hoteli waliyokuwepo na kwenda kwenye shughuli zao.
Ni katika mizunguko hiyo ndipo wakakutana na ajali mbaya ambapo gari lao liligonga lori la mchanga kwa nyuma, ajali ambayo ilitokea katika njiapanda ya Kisauni, Mombasa. Mwenzao alikufa pale pale, lakini Mbaraka na Omar walifia hospitali.
Mbaraka alifariki saa 1.55 usiku baada ya kuwa amepoteza damu nyingi na hakukuwepo na mtu wa kumuongezea damu. Safari yake ikawa imeishia hapo.
Afrika Mashariki yote ilizizima kwa msiba huo. Hata hivyo, mwili wake ulisafirishwa na kwenda kuzikwa kijijini kwao Mzenga, Kisarawe.
Hizi ni baadhi ya albamu alizoshiriki marehemu Mbaraka tangu akiwa na Morogoro Jazz hadi Super Volcano:


Morogoro Jazz Band

Albamu ya ‘Hallo Betty” akiwa na bendi ya Moro Jazz ilirekodiwa katia studio za Chandarana huko Kericho, Kenya mwaka 1968 na 1969. Nyimbo zilizokuwemo ni Jirani Nisaidie, Hallo Betty, Dawa Ya Mapenzi, Niliota Ndoto, Amina Mpenzi, Yameshanichosha, Talaka, Nashangaa, Moro Phata Phata, Furaha Ya Saba Saba na Waloleni Moro.

Masimango ni albamu ambayo ilirekodiwa ikihusisha nyimbo zilizorekodiwa kati ya mwaka 1969 na 1972, zikiwemo 6 kati ya 8 zilizomo kwenye Vol. 3 na baadhi kutoka Vol. 1 na 2.

Super Volcano
Ukumbusho Vol. 1 ni albamu iliyokuwa na nyimbo kama Shida, Nisalimie Wanazaire, Mapenzi Yanitesa, Choyo Uache, Tutakuja Gombana, Dk. Klerruu na Esta Wangu.

Ukumbusho Vol. 2 ilikuwa na nyimbo za Mtaa wa Saba, Pole Dada, Urafiki Mwisho wa Mwezi, Vijana wa Afrika, Kizena, Jasinta, na Sululu ya Moro.

Ukumbusho Vol. 3 ilikuwa na nyimbo kama Mapenzi Shuleni, Daktari Ni Mimi, Wanisikitisha Mpenzi, Nikupendeje, Nirudie Mama, Ushamba Umekutoka, Masimango, Ewe Mwana.

Ukumbusho Vol. 4 ilikuwa na nyimbo za Utanikondesha Maria, Uaminifu Nimeutambua, Mama Chakula Bora, Roho Ndiyo Mwamuzi, Masika Mtindo Mpya, Kasema Hakutaki, Dina Uliapa, Bibi Wa Watu.

Ukumbusho Vol. 5 ilikuwa na nyimbo za Unanitafuta Nini, Nitamtuma Mshenga, Makao Makuu Dodoma, Akula Mwembe Songo, Fadhili Ya Punda, Matamko Ya Viongozi Wetu, Tina Turudiane, Sina Pesa.

Ukumbusho Vol. 6 ilikuwa na nyimbo za Masika Zole Zole, Harusi No.2, Dawa Ya Mapenzi, Afadhali Umerudi, Ugeni Tabu, Kifo Cha Pesa, Mshenga No.2, na Unaulizwa.

Ukumbusho Vol. 7 ilirekodiwa mwaka 1970 mara baada ya bendi hiyo kufanya maajabu katika maonyesho makubwa nchini Japan. Albamu hii ilikuwa na nyimbo kama Regina, Expo 70 Pt 1 & 2, Masikitiko Yetu, Nipeleke Nikashuhudie, Picnic Ya Volcano, Penzi Lako Hatari, Watalii.

Ukumbusho Vol 8 ilikuwa na nyimbo za Mashetani, Safari Siyo Kifo, Baba Mdogo, Mashemeji Wangapi, Matrida Huna Siri na Talaka Kampa Nani.

Ukumbusho Vol. 9 ilikuwa na nyimbo kama Twawapongeza Wanasoka, Kazi Ndiyo Msingi, Regina, Heko U.W.T., Mrudishe, Tunachogombea Nini, Mwongoza Wa Tanu na Ukombozi Wa Afrika.

Ukumbusho Vol. 11 ilikuwa na vibao vya Penzi La Mashaka, The Beat is Mahoka, Pole Dada, Ujamaa Na Kujitegemea, Nasikia Mwaniteta, The Beat is Mahoka II, Esta Wangu, Wana Moro, Nimechoka Kusemwa, Mandhi, Nalilia Raha, Penzi La Mashaka II.

Ukumbusho Vol. 12 ilikuwa na nyimbo za Usiingilie Ugomvi Wao, Poleni Rufiji, Happy Christmas, Huyu Ni Shemeji Yako, Harusi No. 2, Sitakata Tamaa, Headquarters Ya Volcano, Vipi Posa (Mshenga No. 2).


Tazama mashairi ya wimbo wa Mtaa wa Saba:

Sasa nimehamia mtaa wa saba,
Toka pale nilipokuwa nikikaa zamani
Ile nyumba sio nyumba ilikuwa [na mikosi ooh]x2

Nimehama nimehama kuona balaa imezidi
Na kama hauishi ndani ya nyumba iyooo jama
Ndoto ndoto za ajabu haziishi [Tulalapo] x2

Darini hakusemeki mapaka hayeshi kulialia
Usiiu kucha usingizi hauji kabisa
Watoto haweshi kuumwa umwa [eeeeh jamaaa eeh] x2

[Jamaaa]

Kibwagizo:
Maneno; maneno; hakuna
Tunaishi kwa raha sana
Wapangaji hawana zogo nami
Baba mwenye nyumba sina masile naye [Nashukuru MUNGU eeeh]

Hata mwezi sijamaliza oooh
Kazini wakanipandisha na cheo
Watoto na mama yao sasa kuumwa umwa [kote kumekwisha eeeh eeeh eeeh]

[Wote tungekwisha]

Oooooh oooh mama x2 OOOH Lusana oyeeee mamah

Maneno; maneno; hakuna
Tunaishi kwa raha sana
Wapangaji hawana zogo nami
Baba mwenye nyumba sina maneno naye Nashukiuru MUNGU


NB: Unaweza kuwasiliana nami kwa simu +255 715 070109 au brotherdanny5@gmail.com.

No comments