WADAU WATAKA SIKU YA MSANII IAZIMISHWE NCHI NZIMA
Wasanii na wadau wa Sanaa
wameomba kuwe na juhudi za halmashauri na mikoa yote nchini kuunga mkono
maazimisho ya siku ya msanii ambayo yamekuwa yakiadhimishwa kila mwaka hapa
nchini.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti kwenye tathmini ya maazimisho ya Siku ya Msanii maarufu kama Msanii Day
iliyofanyika mapema wiki hii ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
zilizoko Ilala Sharif Shamba wadau hao walieleza kusikitishwa na siku hiyo
muhimu kuadhimishwa mkoa wa Dar es Salaam pekee huku wasanii wa mikoani
wakiachwa nyuma.
“Tanzania ina wasanii wengi,
haiwezekani siku hii muhimu kwao iwe inagusa wasanii wachache tu. Tunaamini
halmashauri na mikoa ina nafasi kubwa ya kuwaunganisha wasanii nchi nzima na
kuunga mkono juhudi za Baraza katika kuadhimisha siku hii” alisema Msanii wa
Sanaa za Maonesho Nkwama Ballanga.
Aliongeza kuwa kupitia
maafisa Utamaduni shughuli za Sanaa zimekuwa zikiendelea maeneo mbalimbali
nchini hivyo lazima kuwe na maelekezo maalum kutoka Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ya kuwataka maafisa Utamaduni
kuwaunganisha wasanii wote katika kuadhimisha siku hii ambayo imekuwa
ikiadhimishwa Dunia nzima huku kila nchi ikiwa na namna yake ya kuadhimisha.
Tunajua wasanii katika
halmashauri zetu wanafanya kazi nzuri sana lakini pia wana changamoto nyingi
zinazowakabili. Kuunga mkono maadhimisho ya siku yao nchi nzima ni kujenga
mfumo wa wao kujipongeza, kujitathimi lakini pia kuonesha kazi zao mbalimbali
kulingana na fani zao” aliongeza Ballanga.
Kwa upande wake Msanii Ahmad
Dadi wa Kundi la Sanaa za Maonesho la Lumumba alisema kuwa siku ya Msanii ni
muhimu katika kutambua na kuthamini mchango wa wasanii mbalimbali nchini hivyo
lazima kuwe na juhudi za makusudi za kuifanya yenye kufana na yenye kumgusa
kila Msanii nchini.
“Tuna wasanii wakongwe ambao
wamefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi. Hii ndiyo fursa ya kuwaonesha wasanii
wa kizazi cha sasa hali ya Sanaa ilivyokuwa. Kuwepo kwa majukwaa ya maadhimisho
kama haya nchi nzima kutaonesha thamani ya Sanaa nay a wasanii” alisema Dadi.
Siku ya Msanii mwaka huu
imepangwa kuazimishwa Oktoba 29 ambapo inatarajiwa kupambwa na shamrashamra
mbalimbali
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO - BASATA
Post a Comment